Kuelekea miaka 60 ya uhuru, Fahamu kuhusu Bibi Titi Mohamed: “Mama wa Taifa” Tanzania

Dondoo: Picha sauti na maudhui ni kutoka dw swahili

Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyesifiwa na kupewa jina la baba wa taifa. Lakini bila ya Bibi Titi Mohamed, asingekuwa na ushawishi wa kutosha wa kufanikiwa kuikomboa nchi hiyo

Bibi Titi alizaliwa lini?

Bibi Titi Mohamed alizaliwa 1926 katikati mwa jiji la Dar es Salaam kwenye familia ya Kiislam. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu rasmi, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa jumla. Katika miaka ya 1950, alikuwa ni miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Uingereza akiwa pamoja na Julius Nyerere, chini ya mwamvuli wa chama cha Tanganyika African National Union, TANU.

Kipi kilimpa umaarufu Bibi Titi Mohamed?

Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye. Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha TANU, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake kuunga mkono maoni na sera za TANU.

Tueleze zaidi kuhusu kupanda na kushuka kwa Bibi Titi Mohamed

Baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Rais Julius Nyerere. Lakini ghafla alipoteza cheo hicho baada ya kutokubaliana na itikadi za ujamaa za Nyerere. Mnamo 1969, pamoja na wenzake sita, miongoni mwao Waziri wa Kazi Michael Kamaliza na maafisa wengine kadhaa wa kijeshi, Bibi Titi alikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kupanga njama za kuipindua serikali. Bibi Titi na wenzake hao walikuwa ni watu wa kwanza nchini Tanzania kukabiliwa na mashtaka ya uhaini. Baada ya kesi kusikilizwa kwa siku 127, Bibi Mohamed alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Hata hivyo, miaka kadhaa baadae aliachiliwa huru mnamo mwaka 1977 baada ya kusamehewa na Rais Nyerere. Baada ya hapo, aliishi maisha ya upweke bila ya familia yake wala marifiki zake aliokutana nao wakati wa harakati zake za kisiasa.

Bibi Titi Mohamed anakumbukwa vipi?

Baada ya kutengana na Julius Nyerere, ikawa vigumu kupata taarifa zozote zinazomhusu Bibi Titi Mohamed. Kwa muda mrefu, serikali ilikaa kimya kuhusu mchango wake na mafanikio yake. Ukosefu huu wa kuutambua mchango wa Bibi Titi Mohamed katika harakati za ukombozi wa Tanganyika unaendana na tabia iliyozoeleka ya kutotambua michango ya wanawake, hasa ya kisiasa inayoandikwa katika vitabu vya historia.

Lakini mambo yalibadilika 1991. Katika chapisho la chama la kuadhimisha miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi alitajwa kama “shujaa wa kike katika harakati za ukombozi”. Moja ya barabara kuu jijini Dar es Salaam imepewa jina lake. Alifariki dunia mnamo mwaka 2000. Watanzania wengi wanamkumbuka kama “Mama wa Taifa”.

Leave a comment