Je, Unashauriwa ufanye nini endapo utapata tatizo la kutokwa na damu Puani?

Utokaji damu wa ghafla puani pasipo kupata jeraha lolote ni tatizo linalojitokeza mara nyingi, hasa kwa watoto kuliko watu wazima.

Tatizo hili likiwapata watoto, wazazi au walezi wengi huwa hawajui nini cha kufanya wanapokutana na hali hiyo kwa watoto wao.

Hata hivyo, tatizo hili mara nyingi halina madhara makubwa, na mara chache hulazimisha mtoto kuwa chini ya uangalizi wa madaktari au wahudumu wa afya kwa muda fulani. Lakini huweza kuleta hali ya wasiwasi kwa wazazi na watoto wenyewe.

Mara nyingi tatizo hili ni suala dogo ambalo linaweza kudhibitiwa kwa njia za kawaida kama vile kugandamiza kwa nguvu sehemu ya nje ya pua pande zote mbili ndani ya dakika 5-10 kwa kutumia kitaambaa safi, pamba au bandeji.

Linapokuwa tatizo sugu njia nyingine saidizi zinaweza kutumika ikiwamo dawa ya matone ya puani ambayo hugandamiza mishipa ya damu na kuzuia damu isivuje.

Njia nyingine ni ya kitabibu zaidi ambayo ni kwa kutumia vitambaa laini na mpira maalumu (balloon catheter)

Watoto wenye tatizo hili linalojirudia mara nyingi ni vizuri wakafanyiwa uchunguzi wa kina, ili kubaini sababu za kujirudia kwa tatizo hilo.

Ingawa yapo mambo yanayoweza kulisababisha ikiwamo majeraha kwenye ukuta wa ndani ya pua, mzio (allergy), maambukizi ya puani, magonjwa ya damu kama vile saratani ya damu, magonjwa ya chembe sahani, homa ya rumatiki pamoja na homa ya matumbo.

Mara nyingi tatizo hili linapotokea kwa watoto, mfumo wa hewa na damu huwa hauathiriki kwa haraka.

Litokeapo mzazi au mlezi kwa haraka anatakiwa kujua hali ya mgonjwa kwa ujumla, anavyoonekana, mapigo ya moyo, upumuaji, na hali yake ya ufahamu. Kama haviko sawa mpeleke katika huduma za afya haraka.Advertisement

Kama yupo kawaida basi mwambie mtoto apenge pua yake na usafishe masalia ya damu kwa kitambaa safi, mkalishe mtoto kwenye kiti na kandamiza pua yake kwa nguvu kiasi kwa muda wa dakika 10, jaribu kumweka mbali na msongamano wa watu.

Endapo mtoto anatapika damu au anacheua damu, uangalizi na usaidizi wa namna ya kupumua kwa mtoto ni vizuri utiliwe maanani.

Endapo mgandamizo wa puani haujasaidia kuzuia damu, lowesha kitambaa cha kotoni kwenye maji ya kawaida yenye chumvi au kama ni hospitalini tumia kimiminika cha salaini na weka kitambaa hicho kwenye sehemu ya nje ya pua na endelea kugandamiza kwa muda wa dakika 15.

Kama njia hizi zimeshindwa kuzuia tatizo hili, haraka sana mtoto apelekwe kwenye kituo cha afya kwa matibabu zaidi. Lakini kabla ya kumpeleka mgonjwa kwenye kituo cha afya, hakikisha unajaza kitambaa safi cha kotoni kwenye matundu ya pua ili kuzuia upotevu wa damu nyingi ukiwa unampeleka kwa daktari.

Mwendelezo wa uwekaji wa vitambaa vya kotoni kwa muda mrefu kwenye pua kuna madhara kwa mfumo wa upumuaji, hakikisha kuviondoa mara tu damu inapoacha kutoka.

Ikumbukwe kuwa damu ni chembechembe zinazoleta uhai kwa mwanadamu, hivyo upotevu mwingi unaweza kuhatarisha uhai wa mtoto endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Hivyo hakikisha unamfikisha haraka katika vituo vya huduma ya afya

Leave a comment