Mjengo Mpya wa Nisha Kufuru!

MJENGO aliozindua staa wa Bongo Movies, Nisha, wikiendi iliyopita, umewasuta mastaa wengi wa Kibongo ambao wanaishi nyumba za kupanga.

Baadhi ya mastaa wa kike wa Bongo Movies wanaotukanwa kutokana na Nisha kuzindua mjengo wake huo wa kifahari ni pamoja na Wema Sepetu, Kajala Masanja, Irene Uwoya na wengine wengi wanaoishi kwenye nyumba za kupanga.

Nisha ameweka wazi nyumba yake aliyoijenga maeneo ya Goba Jijini Dar es Salaam anayodai kumgharimu zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania ambayo anasema ndio imekua ni nyumba ya ndoto yake.

“Ilikuwa ndoto yangu, nilijinyima nikapoteza mpaka mashabiki lengo ilikuwa nikutimiza hili, nimeanza kujenga tangu mwaka 2018 niliponunua kiwanja, unajua Wasanii tunaishi maisha ya kufeki nilichoka kupanga, ramani nimechukua kwenye moja ya mjengo niliowahi kupanga…”

“Wenye nyumba walionipangishaga wamekuja na wamefurahi kuniona na kwangu sasa, nimejenga kwa hela za movie, lakini pia Nishass Wedding vilevile michezo ya kuweka hela na kukopa ya kina Mama imesaidia, kwa wengine hii inaweza kuwa ndogo lakini kwangu ni kubwa sana na nina mshukuru Mungu sana…” Aliandika Nisha na kuongeza;

“Kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu mno kwa zawadi hii aliyonipa maishani mwangu. Pengine ni ndogo kwa wengine ila kwangu ni kubwa mno. Kukatisha na kusimamisha baadhi ya vitu ili tu ndoto zako zitimie haikuwa kazi ndogo kabisa.

“Nilipoteza marafiki, baadhi ya mashabiki n.k nilipoamua kujitoa kwenye spot light na kuishi maisha halisi na ku-focus kwenye future yangu. Nyumba yangu ilikuwa ni zawadi ya birthday yangu, ila Mwenyezi Mungu akapanga leo (Ijumaa iliyopita) ndiyo iwe zawadi yangu.

“Naomba wote mnaotafuta kwa jasho msichoke kupambana Mungu ni wa kwetu sote na anasikia sala zetu. Ahsanteni mashabiki wangu, familia yangu, rafiki, zangu, media zote, kubwa kuliko wateja wangu wa Nishas Wedding kwa kuniwezesha kufanikisha hili. Alhamdullilaah…

Leave a comment